WAFANYABIASHARA wa Mkoa wa Ruvuma wamepitisha azimio la kushiriki kwa mara ya kwanza kwenye maonesho ya Tano ya bidhaa za viwanda vya Tanzania ambayo yanatarajia kufanyika katika viwanja vya Mwl.J.K.Nyerere Dar es salaam kuanzia Desemba 3 hadi 9 mwaka huu.
Azimio hilo limepitishwa katika kikao cha wafanyabiashara wa Mkoa wa Ruvuma kilichoratibiwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) na kufanyika kwenye ukumbi wa SIDO Mkoa wa Ruvuma mjini Songea.
Akizungumza wakati wa ufungaji wa kikao hicho. Katibu Tawala wa Mkoa Stephen Ndaki amewapongeza wafanyabiashara hao kwa kupitisha azimio hilo ambapo amewasisitizia kuwa maonesha hayo ni muhimu kwa kuwa yatapanua wigo wa biashara na kujenga mtandao utakaowapatia masoko endelevu.
Ndaki amesema serikali ya Mkoa wa Ruvuma ipo tayari kuhakikisha kuwa Wazalishaji wa Bidhaa za Viwanda wanatumia kikamilifu fursa adhimu ya kushiriki katika Maonesho ya Tano ya Bidhaa za Viwanda ili kupata teknolojia mpya .
“Soko ni vita,tusizalishe bidhaa na kukaa nazo,kwa hiyo tutoke kutafuta masoko ya bidhaa nje ya Mkoa hivyo ni lazima tuwekeze na tutoke,lengo la serikali ni kuweka mazingira wezeshi ikiwemo kuongeza mitaji,Benki ya Kilimo tumezungumza nao wanakuja Ruvuma unaweza kuunganishwa nao’’,alisisitiza Ndaki.
Ndaki amesema Shirika la viwanda vidogo Tanzania SIDO nao wapo tayari kuongeza mitaji kwa wafanyabiashara ambao wanaweza kutoa mikopo hadi shilingi milioni 500.
Katibu Tawala huyo ametoa rai kwa maafisa biashara katika Halmashauri zote nane mkoani Ruvuma kuwasaidia wafanyabiashara na wajasiriamali ili waweze kushiriki katika maonesho ya bidhaa za viwanda Desemba mwaka huu.
Norah Mishili ni Mwezeshaji kutoka TANTRADE amelitaja lengo la Mamlaka hiyo ni kuona bidhaa zinazozalishwa nchini zinapata masoko yenye tija na njia sahihi inayoweza kukuza na kutangaza bidhaa za wazalishaji.
Amesema wakati wa Maonesho hayo washiriki watapata nafasi ya kujadili na kutatuliwa changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo katika uzalishaji na kuwa na mazingira bora ya biashara.
Naye Afisa Biashara Mkoa wa Ruvuma Joseph Martin ametoa rai kwa wajasirimali wadogo kwenda katika Idara ya Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ili kupata mkopo isiyo na riba ambayo inatolewa kwa vijana,wanawake na wenye ulemavu.
Hata hivyo amesema bidhaa za viwandani,zinahitaji soko la ndani na nje ya Mkoa ambalo linahitaji ushawishi mkubwa hivyo kuna umuhimu wa kushiriki Maonesho ya kimataifa ya bidhaa za viwanda ili kupanua wigo na kupata teknolojia mpya.
kauli mbiu ya ‘Nunua Bidhaa za Tanzania Jenga Tanzania’ inawapa nafasi wenye viwanda kutangaza bidhaa wanazozalisha na kuhamasisha matumizi ya bidhaa hizo kwa jamii nzima hivyo kupanua wigo wa masoko na kujenga uchumi wa nchi.