JOSE Mourinho, Kocha Mkuu wa Tottenham Hotspur amesema kuwa waliadhibiwa jana mbele ya West Ham United kwa kuamini kwamba wamemaliza kazi jambo lililowaponza wagawane pointi mojamoja.
Mchezo huo wa Ligi Kuu England uliochezwa Uwanja wa Tottenham Hotspur, ulikamilika kwa timu zote kufungana mabao 3-3 huku West Ham wakipindua meza zikiwa zimebaki dakika 8 mpira kumalizika kwa kuwa walikuwa wamefungwa mabao matatu mpaka dakika ya 81 .
Spurs ilianza kufunga dakika ya kwanza kupitia kwa Son Heung-min na Harry Kane alitupia mawili dakika ya 8 na 16 na meza ilianza kupinduka dakika ya 82 kupitia kwa Fabian Balbuena na dakika ya 85 Davinson Sanchez alijifunga huku lile la mwisho likifungwa na Manuel Lanzini dakika ya 90+4 na kufanya ubao usome 3-3.
Mourinho ambaye alimtumia mchezaji wake mpya Gareth Bale kwa mara ya kwanza baada ya kurudi kwenye klabu yake hiyo ya zamani akitokea Real Madrid dakika ya 72 akitokea benchi amesema kuwa hafikirii kama anaamini ingeweza kutokea.
"Sidhani kama ningefikiria kwamba inaweza kutokea hali hii lakini kwa kilichotokea tumeadhibiwa kwa kuwa tuliwaadhibu," amesema .