Mkurugenzi wa NEC awaagiza wasimamizi wa uchaguzi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria

Mkurugenzi wa NEC awaagiza wasimamizi wa uchaguzi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria

 

 Mkurugenzi wa Uchaguzi Dkt.Wilson Charles akifungua mafunzo ya uchaguzi kwa wasimamizi wa Uchaguzi wa majimbo Kanda ya Ruvuma Mafunzo ya siku moja ya wasimamzi wa uchaguzi majimbo ya kanda ya Ruvuma yenye mikoa ya Ruvuma,Iringa,Njombe,Mtwara,Lindi na MbeyaBaadhi ya wasimamizi wa Uchaguz wa majimbo Kanda ya Ruvuma wakimsikiliza Mkurugenzi wa Uchaguzi Dkt.Wilson Charles katika ukumbi wa Manispaa ya SongeaPicha ya pamoja wasimamizi wa uchaguzi ngazi ya majimbo mkoani Ruvuma wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Uchaguzi Dkt.Wilson Charles.

***********************************

Mkurugenzi wa Uchaguzi Dkt.Wilson Charles amewaagiza wasimamizi wa Uchaguzi ngazi ya majimbo kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria ili kuepuka malalamiko yanayoweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Dkt.Charles ametoa agizo hilo wakati anafungua mafunzo ya uchaguzi kwa wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo Kanda ya Ruvuma yenye mikoa ya Njombe, Ruvuma,Mtwara,Lindi,Iringa na Mbeya.Mafunzo hayo yamefanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.

“Kama unavyoona Taifa letu sasa hivi kuna baadhi watu  wanachokochoko sana,kwa hiyo mjitahidi kufanya kazi kwa kanuni na sheria za uchaguzi ili kuepuka shari ya watu hao’’,alisisitiza Dkt.Charles.

Amesema hadi sasa NEC imeshatuma sehemu kubwa ya vifaa vya kufanikisha uchaguzi Mkuu ambao unatarajia kufanyika Oktoba 28 mwaka huu na kwamba vifaa hivyo vimekwishaanza kusambazwa na inatarajiwa hadi kufikia Oktoba 24 kila Halmashauri nchini itakuwa imepokea vifaa vyote vya uchaguzi.

Amewashauri wasimamizi wa Uchaguzi katika majimbo kuanza kuvipakua vifaa hivyo na kuvisambaza katika maeneo yote na kwamba wasisubiri hadi Oktoba 27.

“NEC katika uchaguzi wa mwaka huu tunataka kuwa tofauti ukilinganisha na mwaka 2015,kwanza serikali imetuletea fedha zilizotokana na kodi za walipa kodi  kwa wakati,hivi tunavyoongea zaidi ya shilingi bilioni 120 nimezishusha ngazi ya Halmashauri’’,alisisitiza Dkt.Charles.

Amewataka wasimamizi hao kufikisha vifaa vya uchaguzi ngazi ya Kata kwa wakati ili wale ambao wamezoea kulalamika kuwa NEC imechelewa kufungua vituo na kuchelewesha vifaa katika uchaguzi wa mwaka huu wakose cha kusema.

Kwa mujibu wa Dkt. Charles,kuanzia Oktoba 24 hadi 26 NEC itaanza kutoa mafunzo kwa wasimamizi wa vituo,wasimamizi Wasaidizi wa vituo na makarani waongozaji.

“Wasimamizi wa majimbo,mnatakiwa kuyapa umuhimu mkubwa na wa kipekee mafunzo haya hasa kwa kuzingatia kuwa watendaji mtakaowafundisha ndiyo watakaosimamia zoezi la upigaji kura na kuhesabu kura vituoni’’,alisema Mkurugenzi wa NEC.

Dkt.Charles pia amewaagiza wasimamizi wa majimbo kuwaapisha mawakala wa vyama vya siasa ifikapo Oktoba 21 mwaka huu na kusisitiza kuwa  vyama vya siasa ambavyo vitaleta mawakala muda ukiwa umekwisha, mawakala wake hawataapishwa na hawataruhusiwa kuingia kwenye chumba cha kupigia kura.

Mkurugenzi huyo wa NEC amesema daftari la kudumu la wapigakura  lina jumla ya wapigakura milioni 29,188,347 na kwamba katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kutakuwa na vituo 81,567 vya kupigia kura kwa nchi nzima.

Amesisitiza kuwa baada ya wapigakura, kupiga kura zao sheria inawataka  kuondoka vituoni na kurudi nyumbani kusubiri matokeo. na kwamba hakuna sheria inayosema wabaki vituoni.

Gaspar Balyomi ni Msimamizi wa Uchaguzi  Jimbo la Tunduru,akizungumza baada ya kupata mafunzo hayo ameahidi kusimamia maelekezo yote ya NEC ili kuhakikisha wananchi wanapiga kura katika vituo husika kwa uhuru na kurudi nyumbani kusubiri matokeo.

Kwa upande wake Msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Mbinga Mji Grace Quintine amesema mafunzo hayo yamewakumbusha kuzingatia kanuni na sheria za uchaguzi tangu kuanza kwa mchakato wa kuelekea uchaguzi Mkuu.