KAZI ya kuusaka ubingwa imeanza Yanga, hii ni baada ya kocha mpya wa kikosi hicho, Cedric Kaze kuanza kazi rasmi akiwa hataki utani hata kidogo.
Kaze raia wa Burundi, Alhamisi ya wiki hii majira ya saa nne usiku, alitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar, kisha juzi Ijumaa akasaini mkataba wa miaka miwili kuinoa Yanga akichukua mikoba ya Mserbia, Zlatko Krmpotic aliyetimuliwa Oktoba 3, mwaka huu.
Muda mfupi baada ya kupewa mkataba huo, Kaze alifika kambini ilipo timu hiyo pale AVIC Town, Kigamboni jijini Dar na kufanya mazungumzo na vijana wake pamoja na viongozi wenzake wa benchi la ufundi, kisha jana Jumamosi akaanza kuwapigisha tizi vijana wake.
Katika mazoezi ya kwanza jana Jumamosi, Kaze alionekana hataki utani na kazi yake huku akiwaambia vijana wake lazima wafanye mara mbili. Asubuhi na jioni ambapo kila kipindi watakuwa wakifanya si chini ya saa mbili, jumla kwa siku watatumia dakika 240.
Awali Yanga ilikuwa haina ratiba rasmi ya mazoezi ambapo kwa siku wanaweza kufanya mara mbili na siku nyingine mara moja, lakini tangu kocha huyo aelezwe kuwa kwenye mipango ya kutua kikosini hapo, ratiba iliwekwa baada ya timu hiyo kuonekana kuwa na shida kwenye eneo hilo msimu huu.
Baada ya mazoezi ya asubuhi, jioni kazi ikaendelea ambapo tizi lilianza saa 10 na kumalizika saa 12.Akizungumza na Spoti Xtra, Meneja wa Yanga, Hafidhi Saleh, alisema, katika siku yake ya kwanza mazoezini, Kocha Kaze alisisitiza lazima wafanye mara mbili kwa siku. Asubuhi na jioni.
“Kocha ameshaanza kukinoa kikosi leo (jana) akiwa na vijana wake kamili. Mazoezi aliyoanza nayo ni ya kuwaweka fiti wachezaji.
Wachezaji wanaonesha kujituma sana.“Wachezaji wote wapo vizuri isipokuwa Abdulaziz Makame anayesumbuliwa na malaria na Balama Mapinduzi ambaye bado yupo chini ya uangalizi wa madaktari,” alisema Saleh.
KAZE AFUNGUKA
Wakati Yanga kukiwa na uhaba wa mabao huku washambuliaji wao, Michael Sarpong na Yacouba Songne wakishushiwa lawama kutokana na kuchezeshwa mechi nyingi za ligi bila ya mafanikio yoyote, Kaze ameibuka na kuwatetea.
Sarpong na Yacouba, ni wachezaji wapya ndani ya kikosi hicho na tegemeo kwenye eneo la ushambuliaji ambapo kila mmoja amefunga bao moja ndani ya Ligi Kuu Bara msimu huu, Sarpong amecheza mechi nne na Yacouba mechi tano.
“Ngoja nikwambie kitu, Sarpong na Yacouba wote ni washambuliaji wazuri na wanalijua goli vizuri tu, mimi ndiye nilipendekeza wasajiliwe baada ya kuwafuatilia muda mrefu.
“Lakini kilichotokea hadi wanaonekana wachezaji wa kawaida ni kwa sababu walikosa mbinu pamoja na viungo wa kuwawekea pasi za kufunga hali iliyosababisha hayo yote kutokea. Naamini ujio wangu utabadilisha kila kitu na mtauona ubora wao,” alisema Kaze.
KUHUSU UBINGWA
Yanga iliyoukosa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa misimu mitatu sasa ambao umekuwa ukitua Simba, ujio wa Kaze umewafanya wadhamini wao, Kampuni ya GSM kuamini sasa ubingwa msimu huu ni uhakika.
Mkurugenzi Uwekezaji wa GSM ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Usajili Yanga, Injinia Hersi Said, amesema: “Watu ambao nina imani nao kubwa ni kocha wetu Cedric Kaze, huyu atatupa ubingwa, hakuna kitu kingine.“Nina kila sababu ya kusema sisi kwa pamoja tunamuamini Kaze.
Tunachokiomba wanachama na mashabiki kumuunga mkono kocha pamoja na timu yetu kwani tumepata kocha ambaye atatumia elimu na muda wake katika timu yetu. Tumpe muda, tunaamini kutakuwa na mabadiliko makubwa sana.”