Charles James, Michuzi TV
SIKU moja baada ya kuwarudisha CCM wanachama 12 wa Chadema, Mgombea Ubunge Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma CCM, Mariam Ditopile amewarudisha tena wanachama 26 wa chama hicho Kikuu cha upinzani wilayani Bahi, Dodoma.
Wanachama hao wa Chadema wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kata ya Mpamantwa wilayani Bahi, Emmanuel Elias wameomba kujiunga na CCM kwenye uzinduzi wa kampeni za Udiwani za Kata hiyo ambazo zimezinduliwa na Ditopile.
Akizungumza kwenye kampeni hizo Ditopile amesema kwa mambo makubwa yaliyofanywa na Rais Magufuli kwa miaka mitano hasa kwenye Mkoa wa Dodoma ana kila sababu Kwa wananchi wa Bahi kumpigia kura nyingi za heshima ili kumpa nguvu na moyo wa kuendelea kuwatumikia tena kwa miaka mingine mitano.
Amesema kitendo cha Dk Magufuli kuhamishia Makao Makuu na serikali yote Dodoma kimeondoa hata ile adha ya wananchi waliokua na changamoto za ardhi ambazo zimeshindikana kutatuliwa kwenye Halmashauri na hivyo kusafiri umbali urefu hadi Dar es Salaam kwenda wizarani kuonana na Waziri kwani sasa Wizara zote ziko Dodoma.
" Miaka kadhaa nyuma mtu mwenye changamoto yake ya ardhi ingemlazimu kwenda hadi Dar ambapo nauli tu kwenda na kurudi ni Sh 60,000 bado hujala na kulala na hujui utakaa muda gani, leo Serikali ipo Dodoma nauli hadi mji wa kiserikali pale Mtumba kutokea Bahi ni Sh 3,000 hii ni heshima kubwa kutoka kwa Magufuli.
Magufuli ametufanyia makubwa Dodoma hii reli ya kisasa ya SGR imepita hapa Bahi kuelekea Singida wote ambao wamepitiwa na reli kwenye maeneo yao wamelipwa fidia, zaidi ya Sh Milioni 100 zimelipwa kwa wananchi wa Bahi hii ni kuonesha kuwa serikali ya CCM inayoongozwa na Magufuli inajali wananchi wake, twendeni tukampe heshima Oktoba 28 yeye pamoja na Mbunge wa Bahi na Diwani wa hapa Mpamantwa ili wakatufanyie kazi," Amesema Ditopile.
Kwenye sekta ya Afya amesema Magufuli aliahidi kujenga Hospitali kila Wilaya na Bahi imekua mojawapo ya Wilaya zilizonufaika na ahadi hiyo kwa kujengewa Hospitali kwa gharama ya Sh Bilioni 1.7 pamoja na kuwekewa vifaa tiba vya kisasa lakini pia wakinufaika na ujenzi wa vituo vya afya vinne vyenye ubora mkubwa.
Amewaomba wananchi wa kata hiyo kujitokeza kwa wingi Oktoba 28 mwaka huu kwenda kumpigia kura Dk Magufuli ili azidi kuwatumikia na kuboresha maisha ya watanzania kama alivyofanya kwenye elimu ambapo sasa shule ya msingi hadi kidato cha nne wazazi hawalipi ada na badala yake Serikali yake inalipa Sh Bilioni 24 kila mwezi kwa ajili ya elimu bila malipo.
Kwa upande wake Mwenyekiti huyo wa Chadema Kata ya Mpamantwa aliyerudi CCM, Emmanuel Elias amesema kazi kubwa inayofanywa na serikali ya Magufuli ndio iliyomshawishi yeye na wenzake kujiengua Chadema na kujiunga na CCM ili waweze kushirikiana na serikali kuwaletea maendeleo wananchi wao.
" Hivi vitu ni uelewa, leo ndugu Ditopile ametoa darasa kubwa juu ya faida ya serikali kuhamia Dodoma pamoja na mambo makubwa yaliyofanywa na Rais Magufuli, ni kweli tulikua tunapinga tu lakini ukweli wa kazi kubwa inayofanyika tumejionea," Amesema Elias.
Nae mgombea udiwani wa kata hiyo, Sosthenes Mpandu amewaomba wananchi hao kumpigia kura ili akamalizie kazi ambazo alishazianza kwenye awamu yake ya kwanza huku pia akimuombea kura Dk Magufuli na mgombea Ubunge Jimbo la Bahi.
Mgombea Ubunge wa Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma CCM, Mariam Ditopile (kushoto) akimuonesha Aliyekua Mwenyekiti wa Chadema Kata ya Mpamantwa wilayani Bahi, Emmanuel Elias ambaye amejiengua kwenye chama hicho cha upinzani na kurejea CCM.
Mgombea Ubunge Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma CCM, Mariam Ditopile akimvisha tisheti ya CCM aliyekua Mwenyekiti wa Chadema Kata ya Mpamantwa wilayani Bahi, Emmanuel Elias ambaye ameomba kurejea CCM baada ya kuvutiwa na ilani ya chama hicho.
Aliyekua Mwenyekiti wa Chadema Kata ya Mpamantwa wilayani Bahi, Emmanuel Elias (wa pili kushoto) akizungumza mbele ya Mgombea Ubunge Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile kwa niaba ya wenzake baada ya kujiengua Chadema na kuomba kurejea CCM.
Wananchi mbalimbali wa Kata ya Mpamantwa wilayani Bahi ambao wamejitokeza kwenye uzinduzi wa kampeni za Udiwani wa kata hiyo zilizozinduliwa na Mariam Ditopile.
Mbunge wa Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma CCM, Mariam Ditopile akimkabidhi ilani na kumnadi mgombea Udiwani wa Kata ya Mpamantwa wilayani Bahi, Sosthenes Mpandu.