UHURU NA WAJIBU WA VYOMBO VYA HABARI KURIPOTI UCHAGUZI MKUU
Waandishi wa habari wakiendelea na majukumu yao kwenye moja ya mikutano.
Na Kadama Malunde
Tanzania ni mojawapo ya nchi za bara la Afrika zenye idadi kubwa ya vyombo vya habari.
Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) kuna zaidi ya vituo 190 vya redio zikiwemo vituo vya redio vya mtandaoni,vituo vingi vya runinga, zaidi ya vituo 350 vya runinga za mtandaoni, zaidi ya blogu 100 na magazeti zaidi ya 100 yaliyosajiliwa kuripoti taarifa na habari mbalimbali nchini.
Nyongeza ya vyombo hivyo, kukua kwa matumizi ya mtandao wa intaneti nchini kumeongeza idadi kubwa ya njia za kupashana habari na taarifa kupitia mitandao ya kijamii.
Hata hivyo wingi wa vyombo vingi vya habari utakuwa na manufaa tu endapo utahamasisha ushiriki wa wananchi katika kufanya maamuzi na kuchangia mawazo yao kuhusu kujiletea maendeleo.
Aidha, vyombo vingi vya habari vitakuwa na msaada endapo vitafanya kazi katika mazingira wezeshi yanayochochea mawazo kinzani na ushindani wa hoja mbalimbali pasipo kuathiri ulinzi na usalama wa nchi na ustawi wa raia wake.
Ripoti za tafiti za miaka ya hivi karibuni zinatoa taswira ya changamoto ya uwepo wa mazingira wezeshi nchini ambazo, kwa namna fulani zinaathiri uhuru wa vyombo vya habari kuhabarisha jamii kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo uchumi na siasa.
Kwa mujibu wa ripoti hizo, utungaji na utekelezaji wa sheria mbalimbali za vyombo vya habari na kanuni zake imekuwa mojawapo ya changamoto kubwa inayoathiri wajibu wa vyombo vya habari na wanahabari kuwajibika ipasavyo katika misingi ya kiuweledi.
Taifa limeingia kwenye Kampeni za uchaguzi mkuu ambapo wananchi watachagua Rais, wabunge na madiwani, bado kuna sintofahamu ya namna vyombo vya habari vitatimiza wajibu wake kikamilifu kwa kutoa habari za uchaguzi kwa usawa linganifu kwa vyama na wagombea wote kama inavyoelekezwa na sheria za uchaguzi.
Sintofahamu hii inachangiwa na kukosekana kwa maoni kinzani na uchambuzi yakinifu wa taarifa zinazotangazwa na vyombo hivi. Kwa kiasi kikubwa vyombo vya habari na wanahabari wamekuwa waangalifu katika kuchagua na kuripoti aina fulani za taarifa kwa hofu ya kuingia kwenye mgogoro na mamlaka husika.
Pamoja na changamoto zilizopo, bado vyombo vya habari na wanahabari wanao wajibu wa kuripoti taarifa mbalimbali za uchaguzi kwa kuzingatia weledi.
Ni wajibu wa vyombo hivyo kuhakikisha wapiga kura na wananchi wanahabarishwa kikamilifu kwa taarifa zilizofanyiwa uchambuzi wa kina ili kuwawezesha wapiga kura kuchagua kiongozi anayewafaa.
Vyombo vya habari vitoe habari na taarifa zisizoegemea wala kupendelea chama chochote cha siasa na/au mgombea yoyote.
Ni matarajio ya kila Mtanzania kuona kwamba vyombo vya habari na wanahabari wakijielekeza zaidi katika kufanya uchambuzi wa sera na ahadi za vyama na wagombea badala ya kusifia au kushambulia wagombea na kuchochea chuki na mifarakano katika jamii.
Aidha, mamlaka husika zihakikishe uwepo wa mazingira wezeshi na huru yatakayowawezesha wanahabari kutimiza wajibu wao bila hofu, au kuingiliwa na mtu au taasisi yeyote.
Vyombo vya habari vihamasishe ushiriki wa wananchi katika mchakato wa uchaguzi ikiwemo kupaza sauti zao, na kuhoji utekelezaji wa sera na ahadi zinazotolewa na vyama vinavyoshiriki uchaguzi.
Mwezi Oktoba mwaka huu Tanzania inatarajia kufanya uchaguzi mkuu ambapo wananchi watashiriki kuchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Wabunge na madiwani.
Kupitia vyombo vya habari wananchi watapata fursa ya kuwafahamu wagombea na sera za vyama vinavyoshiriki uchaguzi na kuwapima kabla ya kufanya maamuzi kupitia sanduku la kura.