YANGA jana Agosti 30 Uwanja wa Mkapa ilihitimisha kilele cha wiki ya Mwananchi kwa ushindi wa mabao 2-0 mbele ya Klabu ya Aigle Noir ya Burundi.
Mchezo huo ulishuhudiwa na mashabiki wengi waliojitokeza Uwanja wa Mkapa ulikuwa na ushindani mkubwa mwanzo mwisho kwa timu zote kucheza mpira wa darasani na mipango mingi ndani ya uwanja.
Yanga ilianza kuandika bao la kwanza dakika ya 38 kupitia kwa ingizo jipya ndani ya kikosi hicho Tuisila Kisinda akimaliza pasi ya nyota mzawa Feisal Salum ambaye alikuwa ni nyota wa mchezo wa jana.
Aigle walimaliza wakiwa pungufu baada ya mchezaji wao mmoja Koffi Kuassi kuonyesha kadi nyekundu dakika ya 40 baada ya kuonyeshwa kadi mbili za njano dakika ya 10 na ile ya pili ikamfanya mwamuzi asiwe na chaguzo zaidi ya kumuonyesha kadi nyekundu kutokana na kuwa na kadi mbili za njano.
Licha ya wapinzani hao wa Yanga kuwa pungufu bado waliendelea kuwa imara kwa kucheza kwa utulivu huku mipango yao mingi ikiishia miguuni mwa Bakari Mwamnyeto beki mpya wa Yanga aliyesaini dili la miaka miwili akitokea Klabu ya Coastal Union.
Bao la pili kwa Yanga lilipachikwa na mshambuliaji mpya tena wa Yanga, Michael Sarpong ambaye alimaliza kazi ya pasi ya Ditram Nchimbi dakika ya 52 kwa kupiga kichwa kilichozama moja kwa moja nyavuni.
Winga wa Yanga, Farid Mussa amesema kuwa walipambana mwanzo mwisho kwa kuwa walikuwa wanajua wanachotaka huku akiwaomba mashabiki wawape sapoti.
Muangola wa Yanga, Carlos Carlinhos aliingia dakika ya 81 akichukua nafasi ya beki Abdalah Shaibu,'Ninja' na alifanya jaribio moja ambalo halikuzaa matunda.
Wengi walifurahia pia show ya kibabe iliyofanywa na Harmonize, Konde Boy ambaye aliingia kwa mtindo wa kininja uwanjani kwa kutumia kamba ndefu jambo lililwafanya mashabiki wengi wamshangilile mwanzo mwisho.
Licha ya Konde Boy kuanguka wakati wa kushuka uwanjani alionyesha kwamba yeye ni mwamba na yupo imara kwa kufanya onyesho ambalo lilikonga nyoyo za mashabiki wa Yanga pamoja na wadau ambao walifuatilia onyesho hilo lililorushwa mubashara Azam Tv.
Yanga inajiaanda kwa sasa na mchezo wa Ligi Kuu Bara unatarajiwa kuchezwa Septemba 6 Uwanja wa Mkapa itakuwa dhidi ya Tanzania Prisons.