ZLATKO Krmpotic, Kocha Mkuu wa Klabu ya Yanga amesema kuwa amewaona wachezaji wake wakionyesha kiwango bora kwa kila mmoja ila wanahitaji muda wa kuzoeana zaidi.
Zlatko raia wa Serbia amesaini dili la miaka miwili kuinoa Yanga akichukua mikoba ya Luc Eymael raia wa Ubelgiji ambaye alifutwa kazi mazima Julai 27,2020.
Alikishuhudia kikosi chake Agosti 30 kwenye kilele cha wiki ya Mwanachi ambapo Yanga ilishinda mabao 2-0 mbele ya Aigle Noir ya Burundi kwenye mchezo wa kimataifa wa kirafiki..
Mabao ya Yanga yalifungwa na Tuisila Kisinda dakika ya 38 kwa pasi ya Fei Toto na Michael Sarpong dakika ya 52 kwa pasi ya Ditram Nchimbi.
Kocha huyo amesema:"Nimewaona wachezaji kila mmoja ana kitu chake ila kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza bado nina amini wanahitaji muda ili kuwa bora zaidi."
Yanga itafungua pazia la mechi ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2020/21 dhidi ya Tanzania Prisons, Uwanja wa Mkapa, majira ya saa 1:00 usiku Septemba 6.