KUMEKUCHA, SIMBA YATAJA MAJEMBE YATAKAYOPIGWA CHINI NDANI YA KIKOSI

KUMEKUCHA, SIMBA YATAJA MAJEMBE YATAKAYOPIGWA CHINI NDANI YA KIKOSI

UONGOZI wa Simba umetangaza kuwa wachezaji watakaobaki kuendelea kuvaa jezi za timu hiyo msimu ujao ni wale walioonyesha ubora mkubwa msimu huu wa 2019/2020.

Kwa maana hiyo, wachezaji ambao huenda Simba ikaachana nao kutokana na kutotoa mchango mkubwa katika timu hiyo ni Yusuph Mlipili, Tairone do Santos, Rashid Juma, Haruna Shamte na Sharraf Eldin Shiboub.

Wakati timu hiyo ikipanga kutembeza panga hilo, tayari wapo wachezaji wanaohusishwa kujiunga na timu hiyo kwa msimu ujao ambao ni Michael Sarpong, Bernard Morrison na Bakari Mwamnyeto.

Akizungumza na Spoti Xtra, Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa alisema kuwa soka siyo mchezo wa kujificha, wale wachezaji walioonyesha na wasioonyesha ubora wao wameonekana, hivyo benchi la ufundi na uongozi hawatatumia nguvu kuwaondoa kikosini walioshindwa kuendana na kasi ya timu.

Senzo alisema kuwa kazi ngumu ipo kwenye usajili wa wachezaji pekee kwa kutumia ripoti ya kocha wao Mbelgiji, Sven Vandenbroeck ili kuhakikisha wanawapata nyota wanaostahili kuichezea Simba msimu ujao.

Aliongeza kuwa, zipo baadhi ya nafasi zinazohitaji kufanyiwa maboresho kwa kuwasajili wachezaji bila ya kufuata ripoti ya kocha ambazo ni ushambuliaji na safu ya ulinzi ya kati inayoongozwa na Erasto Nyoni, Pascal Wawa na Kenedy Juma.

“Lipo wazi kabisa, wachezaji tutakaobaki nao msimu ujao ni wale walioonyesha ubora msimu huu ambao tayari umemalizika.

“Kikubwa tutakachoangalia ni mchango upi ameutoa mchezaji, hivyo baada ya hapo ndiyo zoezi hilo la kuwatangaza wachezaji wa kuwaacha litaanza kwani ni lazima tuwaache ili wengine wapya waje kuchukua nafasi zao msimu ujao.

“Tumepanga kufanya usajili wenye tija katika timu, lengo ni kuwa na kikosi imara kitakachotupa ubingwa wa ligi, Kombe la FA pia kufika mbali katika michuano ya kimataifa tutakayoshiriki msimu ujao,” alisema Senzo.