HIVI DIVYO YANGA ITAKAVYOMTABULISHA JAMES KOTEI AGOSTI 9, NYOTA WENGINE 9 NDANI

HIVI DIVYO YANGA ITAKAVYOMTABULISHA JAMES KOTEI AGOSTI 9, NYOTA WENGINE 9 NDANI
YANGA imedhamiria kuimarisha kikosi chao kuelekea msimu ujao ambapo mabosi wa Kamati ya Usajili chini ya udhamini wa GSM wameandaa sapraizi kubwa kwa mashabiki wao itakayofanyika katika kilele cha Tamasha la Wiki ya Mwananchi.

Timu hiyo imepanga kukiboresha kikosi chao kwa kusajili wachezaji tisa watakaoingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo msimu ujao.

Tayari wapo baadhi ya wachezaji wanaotajwa kwenye usajili wa timu hiyo, kati ya hao ni kiungo Mkongomani,Mukoko Tonombe anayekipiga AS Vita ya DR Congo, Eric Rutanga (Rayon Sports), Tuisila Kisanda (AS Vita), Heritier Makambo (Horoya AC) na Yacouba Songne ambaye ni mchezaji huru.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, rasmi kilele cha tamasha kubwa la Wiki ya Mwananchi litafanyika Agosti 9, mwaka huu ambapo siku hiyo, Yanga wataitumia kutambulisha wachezaji wao wa msimu ujao wa 2020/21.

Kati ya watakaotambulishwa ni kiungo mkabaji wa zamani Simba, Mghana, James Kotei.Mtoa taarifa huyo alisema kuwa, GSM wamefanikisha usajili huo kwa asilimia mia na kilichobaki ni kiungo huyo kutua nchini kwa ajili ya utambulisho rasmi kwa mashabiki wa timu hiyo, kisha kuanza kazi.

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa, ujio wa kiungo huyo umepangwa kufanywa siri kubwa na mara atakapotua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, kila mmoja ataamini kweli wameamua kukijenga kikosi chao.

Aliongeza kuwa, utambulisho wa kiungo huyo unatarajiwa kuwa wa tofauti na wachezaji wengine wapya watakaojiunga na timu hiyo katika kuelekea msimu ujao.

“GSM kwa kushirikiana na viongozi wa Yanga tayari wamekamilisha usajili wa wachezaji wao wapya kwa asilimia 90, kilichobaki ni nyota hao kuanza kuwasili nchini tayari kwa ajili ya utambulisho.

“Wachezaji hao watatambulishwa Agosti 9, mwaka huu, siku maalum iliyopewa jina la Wiki ya Mwananchi ambayo huitumia Yanga kutambulisha wachezaji wao watakaowatumia msimu ujao.

“Katika siku hiyo ndiyo Kotei atatambulishwa mbele ya mashabiki wa timu hiyo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, pia siku hiyo wachezaji wengine wapya watatambulishwa sambamba na kuingia kambini tayari kuanza msimu mpya,” alisema mtoa taarifa huyo.

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Hassani Bumbuli, alidokeza kuanza mazoezi ya maandalizi ya msimu mpya baada ya wiki mbili kuanzia sasa sambamba na kuanza kushuka kwa wachezaji wapya.

“Kuanzia Agosti Mosi, mwaka huu, mashabiki wa Yanga tarajieni kuanza kuwashuhudia nyota wa kigeni wakianza kutua nchini kukamilisha masuala ya usajili kabla ya kuanza majukumu yao,” alisema Bumbuli.