WANAFUNZI SHULE YA MSINGI DODOMA MLIMANI WAFURAHIA KUANZA MASOMO, WAMPONGEZA RAIS MAGUFULI

WANAFUNZI SHULE YA MSINGI DODOMA MLIMANI WAFURAHIA KUANZA MASOMO, WAMPONGEZA RAIS MAGUFULI
 FURAHA! Kufuatia agizo la Rais Dk John Magufuli kuruhusu masomo yaendelee kuanzia Juni 29, Wanafunzi wa Shule ya Msingi Dodoma Mlimani wameelezea furaha yao ya kurudi shule huku wakimpongeza Rais kwa kuruhusu masomo kuendelea.

Wakizungumza shuleni hapo, wanafunzi hao wamesema waliwakumbuka walimu wao kwa ufundishaji wao mzuri huku wakisema muda wa kucheza kwa sasa haupo zaidi ya kuzingatia masomo.

Wanafunzi hao wanarejea shuleni baada ya miezi mitatu kutokana na serikali kufunga shule na vyuo nchini ikiwa ni jitihada za kujikinga na ugonjwa wa Covid19 unaosababishwa na virusi vya Corona.

Akizungumzia kurejea kwa wanafunzi mashuleni Mwalimu Mkuu wa Shule Teonila Mgulunde amesema anafurahi sana kufunguliwa kwa shule kwani kwa kipindi cha miezi mitatu wanafunzi kukosa masomo kilikua kigumu na imewaumiza kwa kiasi kikubwa.

‘’ Tunaishukukuru sana serikali kwa uamuzi wake huu ,kwani idadi ya watoto waliorudi shuleni ni wengi licha ya kuwa kuna mmoja tumempoteza lakini hakuuumwa ugonjwa huu alikuwa na matatizo mengine, hivyo kwa sasa tunajikita kuwafundisha wanafunzi wetu na kuwaandaa wale wa madarasa ya mitihani," Amesema Mwl Mgulunde.

Jumanne June 16,2020 wakati akitoa hotuba yake ya kuvunja Bunge la 11, Rais Dk John Magufuli alitangaza rasmi kufunguliwa kwa shule zote zilizofungwa kutokana na ugonjwa huo na June 29 ndiyo ilikuwa tarehe rasmi ya wanafunzi kurejea shuleni.

‘’Tuliwakumbuka sana walimu wetu kipindi tulichokuwa nyumbani,muda mwingi umepotea, kwa sasa tumerejea shuleni  sio muda wa kucheza tena, tutasoma kwa bidii na tutafaulu.

Lakini tunamshukuru sana Rais wetu Dk John Magufuli kwa kuamua kuruhusu masomo yaendelee na kututoa hofu kwani amesema hofu nayo husababisha kinga za mwili kupungua," Amesema Hemedi Shaban wa Darasa la Saba.

Naye Elizabelth David ambaye pia yuko Darasa la saba amesema amerejea tena shuleni hivyo atasoma kwa bidii ili aweze kufaulu mitihani yake vizuri.

‘’ Tuliwakumbuka sana walimu wetu,tumekaa nyumbani muda mrefu na hivi sasa tumerejea shuleni nitasoma kwa bidii,nakumbuka wakati niko nyumbani nilikuwa na muda wa kujisomea kupitia madaftari yangu na kupitia runinga kwenye Darasa huru’’ Amesema Elizabeth.

 Wanafunzi wa Shule ya Msingi Dodoma Mlimani wakiendelea na masomo yao kama kawaida baada ya kurejea shuleni kuendelea na masomo yao.