HALMASHAURI WILAYA YA KISARAWE YAAMUA KUWANOA VIJANA KUHUSU SEKTA YA UTALII, JOKATE AWAPA MBINU

HALMASHAURI WILAYA YA KISARAWE YAAMUA KUWANOA VIJANA KUHUSU SEKTA YA UTALII, JOKATE AWAPA MBINU
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani Jokate Mwegelo(aliyesimama)akizungumza leo wakati akifungua mafunzo ya utalii kwa vijana zaidi ya 52 wilayani humo humo ikiwa ni mkakati maalum wa kuandaa vijana kufahamu fursa za utalii kwa maendeleo ya Kisarawe na Taifa kwa ujumla.Kushoto ni Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii Dk.Shogo Sedoyeka na kulia ni Ofisa kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Anna Lawuo

Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii Dk.Shogo Sedoyeka(aliyesimama) akizungumza wakati wa mafunzo ya utalii kwa vijana Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani.Kulia ni Mkuu wa wilaya hiyo Jokate Mwegelo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Kisarawe Mussa Gama akizungumza wakati wa mafunzo ya utalii kwa vijana wa Kisarawe ambayo yamefanyika leo na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa utalii.

Dk.Shogo Sedoyeka ambaye ni Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii akifafanua jambo kuhusu utalii wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya utalii kwa vijana wa wilaya hiyo.Kulia ni Mkuu wa wilaya hiyo Jokate Mwegelo.
Mkuu wa wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani Jokate Mwegelo(kulia) akiwa na wageni wengine waalikwa wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya utalii kwa vijana yaliyoanza leo wilayani humo. 
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo akiwa na viongozi wengine wa halmashauri hiyo pamoja na Chuo cha Taifa cha Utalii wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya utalii yaliyoanza leo kwa vijana 52 wa wilaya hiyo.
Baadhi ya vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe ambao wamepata fursa ya kuteuliwa kwenye mafunzo yanayohusu sekta ya utalii katika wilaya hiyo wakifuatilia kwa makini maelezo mbalimbali kuhusu sekta hiyo na fursa zake.
: Wadau wa sekta ya utalii wakiwemo vijana wanaopatiwa mafunzo ya utalii wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo(aliyevaa suti rangi nyeusi) baada ya kufunguliwa rasmi kwa mafunzo hay oleo Juni 30 mwaka 2020.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo akimuelezea Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii Dk.Shogo Sedoyeka aliyekaa kushoto kuhusu namna ambavyo amebobea katika sekta hiyo ya utalii wakati anazungumza na vijana 52 wa wilaya hiyo ambao wamepata nafasi ya kushiriki mafunzo ya sekta ya utalii ambayo yatafanyika kwa siku tano. 


Na Said Mwishehe, Michuzi TV 

HALMASHAURI ya Wilaya Kisarawe mkoani Pwani imeamua kuandaa mafunzo maalum ya utalii kwa ajili ya vijana wa wilaya hiyo ikiwa ni mkakati wa kuandaa katika sekta hiyo inayokuwa kwa kasi wilayani humo huku wakitakiwa kutumia utalii huo kujiongezea kipato wao na Taifa na kwa ujumla.

Pia Wilaya hiyo imetoa pongezi kwa Rais Dk.John Magufuli kwa uamuzi wake wa kuijenga kwa kiwango cha lami barabara inayopita ndani ya Wilaya ya Kisarawe kwenda Hifadhi ya Taifa Nyerere ambapo wamesema kujengwa kwa barabara hiyo kunakwenda kuimarisha sekta ya utalii kuendelea kupiga hatua kwa kasi kubwa na hivyo kuleta maendeleo kwa wananchi wote.

Akizungumza wakati akifungua mafunzo ya utalii kwa vijana zaidi ya 52 ambao wameanza kupatiwa mafunzo hayo Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo amesema wameamua kutoa mafunzo hayo ikiwa ni mkakati wa kuinua sekta hiyo katika Wilaya hiyo ambayo inavutio vya kila aina.

Jokate amesema kuwa Kisarawe mbali ya kuwa na hifadhi za misitu ya asili pia imebarikiwa kubeba historia yenye kuvutia ikiwemo eneo la Panga la Muingereza, Kibasila, mapango ya popo pamoja na eneo ambalo ukikaa unaiona Rufiji na milima ya Uruguru mkoani Pwani ambapo kupitia mafunzo ambayo yanatolewa kwa vijana hao watapata fursa ya kujivua kwa kina vivutio vilivyopo ndani ya wilkaya hiyo.

“Ni matumaini ya wilaya yetu ya Kisarawe kuwa vijana hawa ambao watakaa hapa kwenye mafunzo kwa siku kadhaa wakitoka watakuwa na uelewa mpana kuhusu utalii na vivutio vyake ndani ya wilaya yetu.Vijana hawa tunataka wawe chachu ya utalii na ndio watakaokuwa wanapokea wageni ambao watakuwa wanapita hapa kwenda hifadhi ya Taifa ya Nyerere,”amesema Jokate.

Amesema huu sio wakati wa vijana kukaa nyuma wakati kuna fursa lukuki za utalii zimewazunguka na kwamba wanataka kuwathibitisha Watanzania kuwa vijana wa Kisarawe wameamka na wapo tayari kuchapa kazi kama ambavyo kauli mbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk.John Magufuli inavyojieleza.

“Hakuna sababu ya vijana kuendelea kubaki nyuma wakati fursa zipo, ni wajibu wetu vijana kila ambacho tunaona kinatuzunguka kukigeuza kuwa fursa, haya mapori yanayotuzunguka tukiyatumia vizuri kiutalii tutapiga hatua na ukweli ni kwamba tunataka Kisarawe isonge mbele itake isitake,”amesema Jokate.







Akifafanua zaidi kuhusu sekta ya utalii amesema Wilaya ya Kisarawe kupitia utalii imekuwa ikipata fedha ambapo kwa sasa imefikia mapato ya Shilingi bilioni 2.7 kutoka shilingi bilioni moja hapo awali.

"Idadi ya watalii wanaokuja Kisarawe nayo imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka na hii inatupa tumaini kuwa vivutio ambavyo tunavyo vinafaida kubwa kwetu, hivyo ni jukumu letu Wana kisarawe kuchangamkia fursa ya utalii ambayo mungu ametubariki.Jumuiya ya Waongoza Utalii ukanda wa Kusini wamepata nafasi ya kuja hapa na hakika wamevutiwa sana na vivutio vyetu,”ameongeza.

Mbali na mafunzo hayo ambayo amewataka vijana hao baada ya kuyapata kutokaa nayo kichwani na badala yake kuyatenda kwa vitendo, amepongeza hatua ya Rais Magufuli kukubali kuijenga barabara ya kutoka kisarawe kwenda Hifadhi ya Taifa ya Nyerere ambapo amefafanua wameipigania kwa muda mrefu na hatimaye leo hii wanaandika historia ya kuwa na barabara ya lami inayoelekea kwenye hifadhi hiyo mpya.

"Tunamshukuru sana Rais wetu Dk.John Magufuli kwa uamuzi wake huu wa kuijenga barabara hii kwa lami, ni barabara ambayo inaelekea hifadhi ya Taifa ya Nyerere na ni fupi zaidi ukipita Kisarawe kwenda kwenye hifadhi hiyo kuliko ukitumia barabara inayopita wilayani Rufuji,”amesema Jokate.

Kwaupande wake Mkuu wa Chuo cha Taifa Cha Utalii.Dkt Shogo Sedoyeka akimetumia nafasi hiyo kuwalezea vijana hao walikuwa kwenye mafunzo kwamba utalii unalipa na kikubwa ni kuendelea kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu utalii ndani ya Wilaya ya Kisarawe ambayo amejiridhisha inavutia kwa utalii.

"Wakati nakuja Kisarawe nimeona kuna fursa nyingi za utalii, hivyo kazi kwenu vijana ambao mnapata mafunzo haya kuchangamkia fursa mara baada ya kumaliza na niimani yangu mtaendelea kujifunza zaidi na zaidi,”amesema Dk.Shogo.

Ametumia nafasi hiyo kuwaeleza vijana hao Chuo watashirikiana na Wilaya hiyo ya Kisarawe ili kuendelea kuelimisha jamii.”Jambo kubwa la kuzingatia katika kumuongoza mtalii ni kuwa mwaminifu,kuonesha tabasamu pamoja na kuyajua kikamilifu maeneo na vivutio vilivyo”.

Wakati huo huo vijana hao wakiwakilishwa na Habiba kulwa na Peter Makayi wamesema katika mafunzo hayo wanaiona pia fursa ya biashara kwani idadi ya watalii itakapokuwa kubwa inakwenda kufungua milango ya biashara kwa wenyeji na hivyo umefika wakati kwa wananchi wa kada mbalimbali kuanza kuweka mikakati ya kufukiria biashara za kufanya.



Habiba Kulwa kwa upande wake amesema huu sio wakati wa kulala kwa vijana wa wilaya hiyo bali wanayo kila nafasi ya kutumia sekta ya utalii kujiinua wao na wilaya kwa ujumla huku akisisitiza umuhimu wa wajasiriamali na wafanyabiashara kuanza kuwekeza kama hatua mojawapo ya kujiandaa kupokea wageni watakaokuwa wanafika kisarawe.



Vijana hao pia wamempongeza pia Rais Magufuli kwa uamuzi wa kuijenga barabara yao inayokwenda hifadhi ya Taifa ya Nyerere kwa kiwango cha lami kwani ni hatua nyingine ya kimaendeleo ya wilaya hiyo na mkoa wa Pwani kwa ujumla.