Njombe DC wavuka tena malengo ya makusanyo ya mapato

Njombe DC wavuka tena malengo ya makusanyo ya mapato
Na Amiri kilagalila,Njombe
Halmashauri ya wilaya ya Njombe ambayo asilimia 70 ya mapato yake inayapata kutoka kwenye mazao ya miti , imefanikiwa kuvuka tena lengo la makusanyo ya mwaka 2019/2020 katika kipindi cha robo tatu ya mwaka kwa kukusanya asilimia 108 ya mapato.
Ripoti hiyo ya makusanyo imetolewa katika kikao cha baraza na mwenyekiti wa halmashauri Valentino Hongoli na kutolewa ufafanunuzi na mkurugenzi Ally Juma ambaye anasema siri ya mafanikio makubwa katika makusanyo yametokana na ongezeko la udhibiti wa mianya ya upotevu wa mapato,Matumizi ya mashine za POS pamoja na kuweka mageti zaidi ya 18 ya ukaguzi na kwamba matarajio ni kukusanya zaidi siku za usoni.
“Upande wa mapato ya ndani pekee halmashauri ilikisia kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 1.8 kutoka vyanzo vya ndani,lakini hadi kufikia mwezi machi 2020 halmashauri imefanikiwa kukusanya kiasi cha bilioni 1.9 sawa na 108% hii inamaanisha halmashauri imefanikiwa tena kuvuka malengo”alisema Valentino Hongoli

Jitihada kubwa za makusanyo ambazo zinatajwa kuchangiwa na uzalishaji mkubwa wa mbao,viazi na mahindi unamsukuma mkuu wa wilaya ya Njombe Ruth Msafiri wakati akitoa salamu za serikali ambapo ameitaka halmashauri hiyo kuanzisha kiwanda cha kuzalisha samani ili kunufaika zaidi na mazao ya misitu badala ya kuuza miti na mbao tu.

“Tunasafirisha mbao nyingi,lakini tunapata hela kidogo sana katika mapato hebu tubadilishe sasa tusafirishe lakini tutengeneze wenyewe,tutainua vijana wajasiriamali ambao tutawjengea kitu kikubwa na itakuwa ni ajira kwao”alisema Ruth Msafiri

Wakibainisha sababu zilizokuwa zikichangia kuwa na upotevu mkubwa wa mapato katika halmashauri hiyo baadhi ya madiwani akiwemo Roida Wanderage na Shaibu Masasi wanasema kipindi cha nyuma kulikuwa na utoroshaji wa mapato na wizi wa fedha za ushuru jambo ambalo limedhibitiwa vyema na matumizi ya mashine za POS.
 Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Njombe Valentino Hongoli wakati akitoa taarifa ya halmashauri na kufungua kikao cha baraza la madiwani.
 Baadhi ya viongozi wakati wakisikiliza hoja za madiwani wakati wa kikao cha baraza la madiwani halmashauri ya mji wa Njombe.
  Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Njombe wakiwa katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa shule ya sekondari Mtwango wilayani Njombe.