NAIBU WAZIRI MGALU AMTAKA MKANDARASI KUMALIZA KAZI KWA WAKATI
Na Ripota wetu – Morogoro
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, amefanya ziara mkoani Morogoro na kumwagiza Mkandarasi, Kampuni ya State Grid, anayetekeleza Mradi wa Umeme Vijijini, mkoani humo kumaliza kazi kwa wakati.
Mgalu alilazimika kufanya ziara hiyo baada ya kupokea malalamiko ya kusuasua kwa Mradi husika ambapo aliwaagiza watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kumsimamia Mkandarasi huyo ili kuhakikisha anakamilisha kazi kwa muda ulioainishwa kwenye Mkataba.
Wakati wa ziara hiyo iliyofanyika Aprili 25 mwaka huu, Naibu Waziri alitembelea baadhi ya vijiji vya Wilaya za Gairo na Mvomero kujionea maendeleo ya kazi husika.
Vijiji vilivyotembelewa ni Ukwamani na Nguyami (Gairo) pamoja na Komtanga (Mvomero). Kadhalika, Naibu Waziri alitembelea Yadi ya Mkandarasi iliyopo Gairo Mjini.
Naibu Waziri aliwaasa viongozi na wananchi wote kwa ujumla kuendelea kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa wa Covid – 19 unaosababishwa na virusi vya Corona huku wakiendelea kufanya shughuli zao.
Pia, aliwataka TANESCO Mkoa wa Morogoro kuhakikisha wananchi wote wanaolipia ili kuunganishiwa umeme, wanapatiwa huduma hiyo kwa wakati.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (katikati-mwenye ushungi), akikagua kazi ya kuunganisha umeme vijijini inayoendelea katika eneo la Ukwamani, wilayani Gairo hivi karibuni.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kushoto), akikagua maendeleo ya kazi ya usambazaji umeme vijijini katika kijiji cha Komtanga, wilayani Gairo, akiwa katika ziara ya kazi, Aprili 25 mwaka huu.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (mwenye ushungi), akikagua Yadi ya Mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Umeme Vijijini, wilayani Gairo, akiwa katika ziara ya kazi hivi karibuni.